Mungu Yuko Wapi Ninapoteseka?
Siku ilianza kama siku nyingine yoyote inavyoanza. Familia ya watu watano walikuwa wanasafiri kwa gari mjini. Ghafla ajali ilitokea. Vyuma, plastiki na miili ya watu vilichanwachanwa. Watu watatu walikufa palepale na wawili walijeruhiwa vibaya sana. Lakini dereva mlevi wa lori lililokuwa linaenda kwa mwendo kasi na ambalo ndilo lililokuwa limewagonga alipata tu michubuko kidogo. Kwa nini?
Dikteta katili anashika hatamu za utawala wa taifa zima, na mamilioni ya watu wanateseka kutokana na matumizi mabaya ya madaraka. Kwa nini?
Daktari anasema, “Nina habari mbaya,” na kisha kwa huzuni anaeleza kuwa una saratani. Kwa nini?
Kila siku visa kama hivi hutokea. Nyakati zingine tunasikia tu habari hizi kutoka kwa mtu fulani au kupitia vyombo vya habari na wakati mwingine habari hizi zinatuhusu sisi wenyewe. Pindi tu tunapotoka kwenye mshtuko huo, hatuwezi kujizuia kuuliza swali lisiloepukika kuliko yote duniani: Kama Mungu ni mwenye uweza wote na ni mwema, kwa nini basi tunateseka? Ni vigumu kufikiria swali kubwa au la muhimu zaidi kuliko hili. Na ukweli ni kwamba, hivi karibuni au baadaye, ipo siku sote tutajiuliza swali hili.
Hutokea kwamba hakuna majibu mengi ya kuweza kuchagua. Tafakari jambo hilo. Ama Mungu yuko tayari kuzuia mambo mabaya yasitokee lakini hana uwezo huo, hivyo si mweza wa yote. Au Mungu anao uwezo wa kuzuia mambo mabaya yasitokee lakini hayuko tayari kuyazuia, hivyo si mwema. Au kuna mtazamo wa tatu: Mungu anaweza na yuko tayari [kuzuia mambo mabaya yasitokee], lakini Mungu ni upendo, hivyo kuna mstari ambao hata Mwenyezi hawezi kuuvuka, na mstari huo ni uhuru wetu wa kuchagua.
Biblia inafundisha mtazamo wa tatu, na ni vigumu kufikiria jibu lingine bora au lenye kufariji zaidi kuliko hili. Kwa ufupi, kisa cha binadamu, kama kilivyoelezewa katika Biblia, kinaelezewa hivi:
- “Mungu ni upendo” (1 Yohana 4:16). Huu ni ukweli wa msingi na muhimu kuhusu Mungu alivyo.
- Kwa hiyo, “Mungu akamwumba mtu kwa mfano wake” (Mwanzo 1:27). Yaani, Mungu aliwaumba wanadamu, wakiwa na uwezo wa kupenda kama Mungu anavyopenda – kwa kutumia hiari yao.
- Na wakiwa wameumbwa na uhuru wa kuchagua na hivyo wenye uwezo wa kupenda, wanadamu “wamefanya dhambi na kuanguka” toka kwenye hali ya utukufu wa kimaadili waliyokuwa nayo baada ya kuumbwa (Warumi 3:23).
- Lakini kuna habari njema: Mungu anatekeleza mpango wa pekee wa wokovu ambao binadamu ye yote na wanadamu wote wenye shauku hiyo wataweza “kuokolewa kwa neema…..kwa njia ya imani” (Waefeso 2:8) – si kwa kulazimisha kwa nguvu, bali kwa uwezo wa upendo wa Mungu unaotuvuta na kutubadilisha. Upendo ndiyo njia pekee ambayo Mungu kwayo anaweza kuangamiza uovu na mateso na wakati huo huo akidumisha uhuru wetu na uwezo wetu wa kupenda.
Je, Hii ni Haki?
Kwa hiyo jibu fupi kuhusu kwa nini tunateseka ni kwamba sisi na wanadamu wengine – siku za nyuma na wakati huu – tumechagua uovu, na mateso ni matokeo ya uchaguzi huo. Hii si haki. Hata haina maana. Kwa ufafanuzi, ni kuwa dhambi si ya haki, ni dhalimu, inaumiza na isiyo sahihi. Dhambi ni ukatili wa wazi. Lakini kuna kitu kimoja ambacho dhambi siyo: siyo mapenzi ya Mungu. Mungu hapendi sisi tuteseke. Wala Mungu hapendi kutufanya sisi watumwa au roboti. Kuwa mwanadamu ni kuwa huru, na kuwa huru inamaanisha kuwa tunaweza ama kuchagua wema au uovu na matokeo yanayohusiana na chaguzi hizo mbili.
Ukweli ulio wazi wa jambo hili ni kuwa upendo hauwezi kuwepo bila ya kuwa na uhuru, na hiari ya kuchagua kwa asili yake huruhusu chaguzi mbaya kufanyika. Kwa hiyo tunaposema kuwa endapo Mungu angekuwa mwema asingeruhusu mtu ye yote kufanya jambo lo lote litakalosababisha maumivu kwake binafsi au kwa mtu mwingine ye yote, huwa tu tunatoa maoni yasiyo na mantiki.
Kinyume chake ni kweli: kwamba kwa sababu Mungu ni mwema, lazima aturuhusu kufanya chaguzi, njema na mbaya, na kupitia uzoefu wa matokeo yake. Daima Mungu anataka tuchague mema peke yake, lakini hatatulazimisha. Mungu kamwe haridhii uovu au mateso ambayo huambatana nao. Sisi wanadamu huwa tunaridhia. Mateso ni matokeo ya uchaguzi wa mwanadamu, sio wa Mungu. Na huo ndio ukweli makini wa uhalisia wa uhuru wetu.
Na bado, Mungu ni mwema mno kiasi kwamba, hawezi kubaki amejitenga mbali au amejikinga dhidi ya mateso yetu. Kulingana na Biblia, Yeye “huchukuliana nasi katika mambo yetu yote ya udhaifu” (Waebrania 4:15). Akizungumzia uhusiano wa Mungu kuhusu maumivu ya mwanadamu, nabii Isaya alisema, “Katika mateso yao yote yeye aliteswa” (Isaya 63:9). Kila mwanafamilia wa jamii ya mwanadamu anapendwa sana na Mungu kiasi kwamba Yesu alisema kuwa lo lote tunalotenda kwa ajili au dhidi ya wenzetu, ni kama kwamba tunamtendea yeye (Mathayo 25:41-45). Mungu huguswa na mateso yote. Anayajua machozi tunayolia na masikitiko yote, huzuni au uchungu unaoambatana nayo. Mfalme Daudi aliimba juu ya huruma ya kina ya Mungu: “Umehesabu kutanga-tanga kwangu; Uyatie machozi yangu yote katika chupa yako; Je! Hayamo katika kitabu chako?” (Zaburi 56:8). Ndivyo upendo ulivyo. Huteseka pamoja na wale wanaoteseka.
Mungu Aliyapitia Maumivu Yetu
Lakini hapa ndipo kisa hiki huzidi kuwa cha kushangaza zaidi. Sio tu kwamba Mungu huhisi maumivu yetu kwenye moyo wake akiwa mbali, kwa waziwazi alijitosa katika maumivu yetu ili kufungua njia ya kuokoka kabisa. Yesu alikuja ili “…aionje mauti kwa ajili ya kila mtu.” (Waebrania 2:9). “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, amejitwika huzuni zetu . . . alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu . . . Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake maovu yetu sisi sote.” (Isaya 53:4-6). Ushahidi mkuu wa upendo wa Mungu katika kukabiliana na maumivu yetu ni kuwa anayeshiriki. Hajatuacha tuteseke peke yetu. Kile kinachomfanya Mungu wa Biblia kuwa wa ajabu kabisa ni kuwa alikuja kwenye dunia yetu kwa hiari yake na alipitia mateso yetu.
Katika jambo lo lote tunalokabiliana nalo maishani mwetu, zipo kweli kuu mbili zisizobadilika ambazo tunaweza kuwa na uhakika nazo: kwanza, Mungu ni upendo na anakupenda wewe binafsi. Na pili, Hatimaye Mungu atasahihisha maovu yote na kuponya majeraha ambayo ulimwengu huu umekupatia. Wakati Yesu alipoteseka na kufa pale msalabani, alithibitisha kuwa Mungu anaipenda zaidi jamii ya binadamu iliyoanguka na inayoteseka kuliko maisha yake na alihakikisha kuwa wote wanaoweka imani katika Yeye watakuwa na mustakabali wenye utukufu usiokuwa na mateso kabisa.
Ahadi ya Biblia, ambayo inathibitishwa na kifo cha Kristo pale msalabani, ni kwa ajili yako: “Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwepo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwepo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita. (Ufunuo 21:4)