Uibukaji Hauwezekani
Maelezo ya uibukaji kwa ajili ya aina zote mbalimbali za uhai hapa duniani hayawezekani. Hii ni imani ya idadi inayoongezeka ya wanasayansi ambao wako tayari kuchukua hatua ya kijasiri ya kusema hivyo. Zifuatazo ni sababu nne kuu miongoni mwa zingine nyingi za kukataa mabadiliko ambayo yaliandikwa na mwanasayansi na mwandishi John F. Ashton MSc, PhD.
Mabadiliko Yasiyowezekana
Wanasayansi leo bado hawawezi kuonesha ushahidi unaodhihirisha kuwa mabadiliko makubwa yatokanayo na uibukaji hata yanawezekana. Sasa baadhi ya wasomaji tayari wanaweza kuwa wanafikiria—subiri, wanasayansi wanashuhudia uibukaji ukitokea. Kweli, tunaona mabadiliko madogo kwa wanyama ambao wameendana na mazingira yao. Lakini utakuta mabadiliko hayo wakati wote yakitoa aina hiyohiyo tu au inayofanana ya mnyama au mmea. Inaweza kuwepo tofauti ndogo katika umbo au rangi. Inaweza kuwa na tofauti ndogo ya kikemikali. Tunaweza hata kutambua kuwa ni mnyama au mmea tofauti—lakini bado ni aina ileile ya kiumbe.
Wanasayansi sasa wanaelewa mabadiliko haya yanafanyika ama kama matokeo ya badiliko katika DNA ya kiumbe au kwenye sehemu ya mfumo wa DNA unapowashwa au kuzimwa. DNA ni molekyuli kubwa sana ambayo hubeba ndani yake michakato muhimu kwa kiumbe kuweza kuishi na kuzaliana. Endapo sehemu ya mfumo huu utabadilishwa, unaweza kusababisha mabadiliko ya kimaumbile—ambayo karibu kila mara huwa na madhara. Wengi wanaoshikilia dhana za uibukaji huamini kwamba, endapo muda mrefu wa kutosha ukiruhusiwa, mabadiliko madogo kama hayo huweza kuibua viumbe tofauti kabisa vyenye viungo vya mwili vipya na tofauti, hivyo kuleta “aina” mpya ya wanyama na mimea. Lakini licha ya madai ya makala nyingi za mazingira asili na vitabu vya sayansi, aina hii ya badiliko kwa kiwango chochote kikubwa haijawahi kushuhudiwa.
Ni kweli kwamba mabadiliko madogo yenye manufaa ya jeni moja wakati mwingine huweza kutokea. Mfano halisi wa hili unaonekana katika viumbe vidogo kabisa ambavyo kupitia mabadiliko yatokeayo bila utaratibu vilizalisha kimengenya kiitwacho nylonase. (Hii huwawezesha kumengenya nailoni kama chanzo cha chakula). Ingawaje, nylonase ni protini rahisi, ambayo haiwezi hata kulinganishwa na kiwango au kiasi cha mabadiliko makubwa sana ya DNA yanayohitajika kwa samaki kubadilika kuwa amfibia—au mabadiliko yoyote makubwa kwa viumbe.
Sio tu suala la kuwa na muda wa kutosha ili mabadiliko mengi madogomadogo yajikusanye. Hata hatua ndogo kabisa zingehitaji mabadiliko makubwa sana ya jeni kiasi kwamba wanasayansi wengi waaminifu wamefikia uamuzi kuwa kuna uwezekano mdogo sana kiasi cha kutowezekana kabisa—na hii ndiyo tathmini yao linapokuja suala la hatua ndogo kabisa za mabadiliko! Zaidi ya hayo, DNA ina uwezo wake wenyewe kiutendaji wa ndani uliokusudiwa kupunguza mabadiliko makubwa. Kwa kweli DNA imeundwa ili kuzuia uibukaji wa aina mpya ya kiumbe.
Tunapofikiria juu ya aina mbalimbali za kushangaza za viumbe hai leo—tumegundua kiasi cha viumbe idadi takriban milioni mbili—pamoja na kadiri ya aina milioni 100 hadi milioni 200 tofauti za viumbe walioishi zamani, kila kiumbe kikiwa na aina ya kipekee ya mfumo wa DNA, tunapaswa kujiuliza swali: Nini chimbuko la mfumo tata wa DNA zote hizo ambao huzalisha viumbe changamani kiasi cha kustaajabisha na mazingira ya kutegemeana kwa viumbe hawa tunayoona?” Hakuna ushahidi wowote kabisa kwamba mabadiliko yatokeayo bila mpangilio yanaweza kuzalisha taarifa tata zinazoweza kusababisha utendaji wa hali ya juu wa mfumo wa mabawa ya wadudu na ndege, mifumo ya uzazi ya wanyama, na mifumo ya mawimbi ya sauti ya popo na nyangumi—achilia mbali akili ya mwanadamu.
Mifumo ya Kukadiria Umri
Swali linalofuata. Je, mabaki ya viumbe hai yana umri gani? Baadhi ya mbinu za za kijiolojia za kukadiria umri (rediometriki) hutoa kiwango cha mamilioni mpaka mamia ya mamilioni ya miaka kwa miamba inayozunguka mabaki ya viumbe hai. Lakini tunapozichunguza taarifa hizo, tunagundua kuwa kupima umri wa matabaka ya mwamba kunaweza kuleta umri tofauti kabisa kutegemeana na njia iliyotumika. Kwa mfano, aina fulani ya mwamba kule kwenye Korongo Kuu lijulikanalo kama Grand Canyon unakadiriwa kuwa na umri wa miaka milioni 516, miaka milioni 892, miaka milioni 1,111, miaka milioni 1,385 na miaka milioni 1,588 kutegemeana na njia iliyotumika. Hivyo ungeweza kusema mwamba huo ulikuwa na umri gani?
Miamba ya Volkano iliyotokea mnamo miaka ya 1950 kwenye mlipuko wa New Zealand ilipimwa kwa njia ya kisasa ya kukadiria umri ya rediometriki. Ingawa miamba hii ilikuwa inajulikana kuwa na umri wa miaka 50 tu, njia hiyo ya kupima umri ilitoa umri ulioanzia miaka mamia ya mamilioni mpaka kwenye maelfu ya mamilioni ya miaka.* Endapo njia hizi huipatia miaka mingi miamba ya hivi karibuni, tunaweza kujuaje kwa hakika umri wa mwamba wowote?
Ukadiriaji wa umri kwa njia ya Kaboni-14, njia pekee ambayo kwa kweli hupima umri wa mabaki ya viumbe hai (na sio tu miamba iliyo kando yake), inaonekana kuwa njia pekee iliyo sahihi zaidi. Inaweza kutoa umri katika kiwango cha maelfu tu (badala ya mamilioni) ya miaka. Uvumbuzi wa hivi karibuni wa tishu laini na vipande vya DNA katika mabaki ya viumbe hai, ikiwa ni pamoja na mabaki ya dinosaria yanayodhaniwa kuwa na umri wa maelfu ya miaka, huunga mkono umri unaopatikana kwa njia ya Kaboni-14 wa miaka maelfu tu kwa mabaki ya viumbe hai.
Seli
Mwisho, ushahidi mpya uliopo sasa huonesha kuwa haiwezekani kwa uhai kuanza wenyewe. Wakati mwingine huliita jambo hili abayojenesisi—yaani, kuibuka kwa uhai kikemikali kutokana na vitu visivyo uhai. Seli hai moja ya kwanza ingehitaji mamia ya aina mbalimbali za molekyuli kubwa, zikiwemo kampaundi za mfumo wa jeni (RNA na/au DNA) ili kujitengeneza. Molekyuli hizi ni ngumu kama sio kwamba haiwezekani kutengenezwa kwenye maabara achilia mbali kujitengeneza yenyewe kwa njia ya asili—na nyingi sana haziko imara, zinavunjika kwa urahisi na kuwa kampaundi ndogondogo zaidi zisizotenda kazi. Aidha, nakala mamilioni za baadhi ya molekyuli hizi zingelihitajika mkusanyiko wa kutosha ili kusababisha mamia ya mabadiliko ya kikemikali kwenda kwenye mwelekeo sahihi kwa mwendo sahihi—ili kuwa na uhai.
Mfumo wa kimahesabu unaonesha kuwa jambo hili haliwezekani kabisa kutokea kwa bahati tu. Kwa kweli, kama tukichukua bakteria hai aina ya E-coli mwenye seli moja na kutoboa tundu dogo katika utando wake wa nje, mchakato wake wa kikemikali utavurugika sana kiasi kwamba seli hiyo itakufa. Zaidi ya hayo, hakuna mwanadamu anayeweza kurejeshea uhai wa bakteria huyo. Vijenzi vyote vya kikemikali bado vipo, lakini hatuwezi kuanzisha tena mamia ya michakato ya kikemikali kwa pamoja katika hali hiyo isiyo na ulinganifu—sharti linalohitajika ili kufanyika kwa uhai.
Tunapofikiria maarifa ya kisayansi tuliyonayo kuhusu uhai duniani, tunaweza kusema kwa hakika kuwa uibukaji peke yake kama chanzo cha aina mbalimbali za viumbe hai duniani ni jambo lisilowezekana kabisa. Badala yake, sayansi hudhihirisha uthibitisho wa mbunifu mwenye maarifa ya kushangaza sana akifanya kazi angalau kwenye kiwango fulani. Kwa nini tusifikirie kile ambacho Biblia Takatifu inadai? Mungu Muumba mwenye upendo aliiumba dunia yetu, lakini adui, aitwaye Shetani, amekuwa akitafuta kufuta ushahidi wa matendo Yake ya uumbaji? Biblia haishii hapo. Si tu kuwa Mungu alipanga juu ya uwepo wako, kitabu cha mwisho cha Biblia, Ufunuo, hudai kwamba ana mpango wa dunia iliyoumbwa upya yenye furaha ya milele kwa ajili yako.