Ahadi ya Amani
Unahitaji amani—Msamaha na amani na upendo wa Mbingu. Fedha haziwezi kuinunua, akili haiwezi kuipata, hekima haiwezi kuileta; huwezi kamwe kuitumainia kuipata kwa nguvu zako mwenyewe. Lakini Mungu anaitoa kwako kama zawadi “bila fedha na bila thamani” (Isaya 55:1). Ni yako ikiwa tu utaunyoosha mkono wako na kuishika. Bwana anasema, “Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu” (Isaya 1:18). “Nami nitawapa ninyi moyo mpya, Nami nitatia roho mpya ndani yenu” (Ezekieli 36:26).
Umeungama dhambi zako, na kwa dhati kabisa umeziweka mbali. Umeamua kujitolea kwa ajili ya Mungu. Sasa mwendee Yeye, na umwombe kwamba akuoshe dhambi zako na akupatie moyo mpya. Halafu amini kwamba anafanya hivi kwa kuwa ameahidi kufanya hivyo. Hili ndilo somo ambalo Yesu alilifundisha alipokuwa duniani, kwamba zawadi ambayo Mungu anatuahidi, lazima tuamini kuwa tunaipokea, kisha huwa yako. Yesu aliwaponya watu magonjwa yao walipokuwa na imani juu ya nguvu Zake; aliwasaidia kwenye mambo waliyoweza kuona, hivyo akawahamasisha kuwa na imani juu Yake kuhusu mambo ambayo hawakuweza kuyaona—akiwaongoza kuuamini uwezo Wake wa kusamehe dhambi. Hili alilisema waziwazi alipomponya mtu aliyekuwa na ugonjwa wa kupooza: “Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza) Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako” (Mathayo 9:6). Vivyo hivyo Yohana, akizungumzia miujiza ya Kristo anasema, “Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina Lake” (Yohana 20:31).
Kuitendea Kazi Ahadi
Kutokana na mfano rahisi wa Biblia jinsi Yesu alivyowaponya wagonjwa, tunaweza kujifunza jambo fulani kuhusu namna tunavyoweza kumwamini kwa ajili ya msamaha wa dhambi. Hebu tuangalia tena kisa cha mtu yule aliyekuwa amepooza kule Bethsaida. Mgonjwa yule maskini alikuwa hajiwezi; alikuwa hajatumia miguu yake kwa miaka thelathini na nane. Lakini, hata hivyo, Yesu alimwamuru, “Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende.” Mgonjwa huyu angeliweza kusema “Bwana ikiwa utaniponya, nitatii neno Lako.” Lakini, hapana, aliliamini neno la Kristo, aliamini kuwa alikuwa ameponywa na akafanya jitihada mara moja; alitaka kutembea na alitembea. Alitenda kwa kulifuata neno la Kristo, na Mungu akampatia uwezo. Aliponywa, akawa mzima.
Kwa namna hiyohiyo wewe pia u mdhambi. Huwezi kulipia fidia ya dhambi zako za nyuma; huwezi kuubadilisha moyo wako na kujibadilisha kuwa mtakatifu kwa uwezo wako mwenyewe. Lakini Mungu anaahidi kukufanyia haya yote kupitia Kristo. Unaiamini ahadi hiyo. Unaungama dhambi zako na kujikabidhi kwa Mungu. Una nia ya kumtumikia. Mara kwa hakika unapotenda hivi, Mungu atatimiza neno lake kwako. Kama unaliamini ahadi,—amini kuwa umesamehewa na umetakaswa,—Mungu hukamilisha jambo hili; umeponywa, kama Kristo alivyomwezesha kutembea yule aliyekuwa amepooza wakati alipoamini kwamba alikuwa ameponywa. Inakuwa hivyo kama ukiamini.
Usisubiri mpaka uhisi kuwa umeponywa, bali sema, “naamini hivyo; nimeponywa, si kwa sababu nahisi hivyo, bali ni kwa sababu Mungu ameahidi.” Yesu anasema, “Kwa sababu hiyo nawaambia, Yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu” (Marko 11:24). Kuna sharti kwenye ahadi hii—kwamba tuombe kulingana na mapenzi ya Mungu. Lakini ni mapenzi ya Mungu kututakasa kutoka dhambini, kutufanya tuwe watoto Wake, na kutuwezesha kuishi maisha matakatifu. Hivyo tunaweza kuomba baraka hizi, na kuamini kuwa tunazipokea, na kumshukuru Mungu ya kuwa tumezipokea. Ni haki yetu kumwendea Yesu na kutakaswa, na kusimama mbele ya sheria bila ya aibu wala hatia. “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu” (Warumi 8:1).
Tangu sasa na kuendelea wewe si mali yako mwenyewe; umenunuliwa kwa thamani. “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwanakondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo” (1 Petro 1:18, 19). Kupitia tendo hili rahisi la kumwamini Mungu, Roho wa Mtakatifu ameumba maisha mapya moyoni mwako. Wewe sasa ni kama mtoto aliyezaliwa ndani ya familia ya Mungu, Naye anakupenda kama vile Mungu anavyompenda Mwanawe.
Njoo Jinsi Ulivyo
Sasa kwa kuwa umekwishajitoa kwa Yesu, usirudi nyuma, usijitenge Naye, lakini siku kwa siku sema, “Mimi ni wa Kristo; Nimejitolea kuwa Wake;” kisha mwombe akupatie Roho Wake na akulinde kwa neema Yake. Kama ilivyo kwa kujitolea wewe mwenyewe kwa Mungu, na kumwamini, ndipo unakuwa mtoto Wake, hivyo ndivyo unavyopaswa kuishi ndani Yake. Mtume Paulo anasema, “Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika Yeye” (Wakolosai 2:6).
Baadhi hudhani lazima wawe kwenye kipindi cha matazamio, na lazima wamdhibitishie Bwana kuwa wameongoka, kabla hawajadai baraka Yake. Lakini wanaweza kudai baraka ya Mungu hata sasa. Lazima wapate neema Yake, Roho wa Kristo, kusaidia udhaifu wao, vinginevyo hawawezi kuupinga uovu. Yesu anapenda tuje Kwake jinsi tulivyo, wadhambi, tusiojiweza, na tukiwa wategemezi. Tunaweza kuja na madhaifu yetu yote, makosa yetu, dhambi zetu, na kuanguka katika miguu Yake kwa huzuni. Ni utukufu Wake kutubeba kwenye mikono ya pendo Lake na kutufunga vidonda vyetu, kututakasa na udhalimu wote.
Hapa ndipo maelfu wanaposhindwa; hawaamini kuwa Yesu mwenyewe huwasamehe, wao binafsi, mtu mmojammoja. Hamwamini na kumtii Mungu kama alivyosema kwenye neno la Mungu. Ni upendeleo kwa wale wote wanaotimiza masharti kujua kwamba msamaha hutolewa bure kwa kila dhambi. Ondoa mashaka kwamba ahadi za Mungu hazikukusudiwa kwa ajili yako. Zipo kwa ajili ya kila mkosaji anayetubu. Nguvu na neema vimetolewa kupitia Kristo ili viletwe na malaika wahudumuo kwa kila roho anayeamini. Hakuna ambaye ni mdhambi kupita kiasi cha kutoweza kupata nguvu, usafi, na unyofu katika Yesu, aliyekufa kwa ajili yao. Anangojea kuwavua mavazi yao yaliyochafuliwa na kunajisiwa na dhambi, na kuwavisha mavazi meupe ya haki; anawasihi waishi, wasife.
Tazameni juu, ninyi wenye mashaka na kutetemeka; kwa kuwa Yesu anaishi ili kufanya upatanisho kwa ajili yetu. Mshukuruni Mungu kwa zawadi ya Mwanawe mpendwa na omba kwamba asiwe amekufa bure kwa ajili yako. Roho anakualika leo. Njoo kwa Yesu na moyo wako wote, na unaweza kudai baraka Yake.
Kadiri unapozisoma ahadi hizo, kumbuka kuwa zinadhihirisha upendo na huruma usioelezeka. Ule moyo mkuu wenye upendo tele unavutwa kuelekea kwa mdhambi kwa huruma isiyo na mpaka. “Katika Yeye huyo, kwa damu Yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema Yake” (Waefeso 1:7). Ndiyo, amini tu kuwa Mungu ni msaidizi wako. Anataka kurejesha sura Yake ya maadili ndani ya mwanadamu. Kadiri unamvyosogelea Yeye kwa maungamo na toba, atasogea karibu na wewe akiwa na rehema na msamaha.
*Imeandaliwa kutoka katika kitabu cha Njia Salama (Steps to Christ, Amani katika Dhoruba, Hatua za Ushindi.