Je, Mungu Anajali Kwamba Ninaumia?

Tunaishi kwenye ulimwengu ambao mambo ya kutisha huwapata watu wasiyoyastahili. Dhoruba hubomoa mabwawa—na maelfu hufa; mamia ya maelfu hawana malazi au maji ya kunywa. Nyumba na mali vimefagiliwa mbali. Au maumivu yanaweza kuwa ya hali ya kawaida—ugonjwa wa ghafla, ajali, talaka, kifo cha mwenzi au mtoto. Kwa sababu yoyote ile, tunalia pale tunapoumizwa. Tunataka kujua, kwa nini? Kwa nini mimi? Je, hivi Mungu anajua—au anajali—wakati mimi ninaumia?

Hata Yesu alikuwa na swali kama hili alipokuwa hapa duniani. “Mungu Wangu, Mungu Wangu,” alilia alipokuwa ameangikwa msalabani, “Mbona umeniacha?” (Marko 15:34). Alijiuliza iwapo Baba Yake alijua—na endapo anajali—kwamba alikuwa akiumia sana kiasi ha kutisha. Biblia humwelezea Yesu kama “Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko” (Isaya 53:3).

Mungu yuko karibu—hata unapoumia

Inawezekana isiwe rahisi kwako kuamini hivi sasa wakati maumivu ni makali mno, lakini Mungu anayajua yote. Na anajali. Yuko karibu sana, hata anapoonekana kana kwamba yuko mbali sana. Tunafahamu kuwa hili ni kweli kwa sababu Yesu aliahidi, “Mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari” (Mathayo 28:20). Mungu yuko pamoja nawe unapoumia. Anasema, “Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha” (Isaya 43:2). Mungu yupo pale kwenye majaribu na maumivu yetu makali sana. Lakini kama hilo ni kweli, kwa nini hafanyi jambo fulani kwa ajili ya kulishughulikia hilo? Kwa nini hayaondoi maumivu?

Kwanza kabisa, unajuaje kwamba Mungu hafanyi jambo fulani katika kukabiliana na maumivu haya? Je, unajuaje kwamba hali yako haingekuwa mbaya zaidi ya ilivyo sasa—bila Mungu kuingilia kati? Tunaishi katika ulimwengu ambao uovu upo kila mahali kutuzunguka. Biblia inasema kwamba uovu huu ni matokeo ya moja kwa moja ya Shetani, ambaye anapingana na Mungu. Lakini taswira katika Biblia hutuonesha kuwa Mungu anauzuia uovu huu—anaukinga usifanye ubaya wake mkubwa zaidi. Kitabu cha Ufunuo huelezea kwa uwazi malaika wanne wanaoshikilia pepo kuu nne za dunia, na malaika kutoka mbinguni anawasihi sana kwamba wasiziachie hizo pepo ziidhuru nchi. Ujumbe hapa ni kwamba Mungu anatulinda dhidi ya athari mbaya kabisa shauku ya Shetani ya kutudhuru.

Changamoto ya Mungu

Jambo la pili, Mungu anayo changamoto. Unaona, tunaishi katika ulimwengu ambao uovu ni uhalisia wa kutisha. Shetani yuko katika mapambano makubwa dhidi ya Mungu na wema. Anajaribu kutuangamiza na kuondoa kila kitu kiletacho furaha. Mungu ana nguvu kuliko Shetani, na mwishowe atashinda katika pambano hili. Dhambi na uovu na maumivu vitatokomezwa kabisa toka duniani na ulimwenguni kote—siku moja fulani. Lakini kwa wakati huu, Shetani anao uwezo wa kusababisha maumivu na madhara na kifo.

Changamoto inayomkabili Mungu ni hii: Jinsi ya kukabiliana na Shetani kwa namna ambayo mimi na wewe tunaweza kuwa na uwezo wa kuchagua pande kwa uhuru? Unaona, uhuru wetu wa kuchagua—ama wema au uovu—ni uhuru wa msingi sana ambao lazima Mungu auhifadhi kwa gharama zote. Kama hatuchagui kuwa upande wa Mungu kwa sababu tunataka kufanya uchaguzi huo kwa uhuru, basi Shetani atakuwa ameshinda. Hapo mwanzo alimshutumu Mungu kuwa ni dikteta na dhalimu katika kudai utii. Alijiweka juu kuwa kama Mungu.

Kwa nini Mimi?

Ni suala la kawaida kuuliza, “Kwa nini mimi?” wakati maumivu na taabu vinapokuja maishani mwako. Mara nyingi huonekana kuwa si haki kabisa. Kwa nini maisha ya baadhi ya watu yanaonekana kutokuwa na maumivu, wakati ambapo mambo ya kutisha yanawatokea wengine? Katika ajali moja, baadhi wanaweza kuondoka bila kuumia, huku wengine wakipoteza maisha yao. Kwa nini? Kwa nini Mungu anaonekana kana kwamba anawatendea miujiza baadhi ya watu—lakini si kwa wengine?

Majibu ya kuridhisha kabisa kwa maswali kama hayo hayapo. Lazima tukumbuke, hata hivyo, kwamba mwisho, nguvu ya miujiza—na sababu ya miujiza hiyo kutokea—inabaki mikononi mwa Mungu, na Mungu peke Yake. Anaiona hali hiyo yote kamili, na atafanya mambo yote kuwa sawa. Anasema mwandishi mmoja wa Biblia, “Mungu yuko mbinguni, na wewe upo chini, Kwa hiyo maneno yako na yawe machache” (Mhubiri 5:2).

Katika hali kama hiyo, lazima tuamini kwamba Mungu anayafahamu majibu, hata kama hatujui, na kuwa hatutafahamu mpaka tutakapoweza kumwuliza ana kwa ana mbinguni. Tunaweza kuamini tu kwamba wakati kumbukumbu zote za maisha hapa duniani zitakapofungwa—wakati tutakapoitazama tena dunia tukiwa mbinguni—tutaridhika kwamba “mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu” (Warumi 8:18).

Jibu la Mungu dhidi ya shambulizi la Shetani lilikuwa kuonesha tabia Yake kamili ya kutokuwa na ubinafsi kabisa kwa kumtuma Mwanawe pekee kuja duniani kuishi kama mmoja wetu na kutufia msalabani.

Sasa, lazima mimi na wewe tuchague kati ya Mungu na Shetani. Na ili kuthibitisha madai ya uongo ya Shetani kwamba Mungu anatulazimisha kumfuata kwa uwezo Wake wenye nguvu, lazima Mungu ahakikishe kuwa uchaguzi tunaoufanya ni wetu sisi wenyewe—kuwa ni wa uaminifu na unafanywa kwa hiari. Ndiyo sababu uhuru wetu wa kuchagua ni muhimu sana kwa Mungu. Lakini pia ndio chanzo cha changamoto ya Mungu. Kwa sababu kama tunaweza kuchagua kwa uhuru, basi tunaweza kuchagua uovu; tunaweza kuchagua kufanyiana mambo ya kutisha sana.

Matumizi mabaya ya Uhuru

Haipaswi kutushangaza, basi, kuwa baadhi ya watu huchagua kufanya uovu, na maumivu na mateso hutokea. Wakati mama kijana anapokufa kwa saratani, wakati ndoa inapovunjika, wakati ajali ya gari inapomwua mtoto—wakati unapoumia kwa sababu yoyote ile—humaanisha kuwa Shetani bado anapambana na Mungu na wakati mwingine Shetani anashinda vita.

Hata hivyo, Biblia hutuhakikishia kwamba mwisho wa yote Mungu atashinda vita. Kitabu cha Ufunuo huelezea jambo hili kwa kutumia taswira imwoneshayo Yesu akiwa amempanda farasi mweupe akiongoza jeshi la mbinguni. Mabilioni na mabilioni ya malaika watakatifu wanamfuata. Uvumilivu Wake kwa uovu wa Shetani umefikia kikomo. Pambano ni fupi. Shetani na wafuasi wake wote waovu wametekwa. Uangamivu wa uovu utakamilika wakati Shetani atakapoharibiwa. Utakuwa Mwisho wa chuki, ukatili, ugaidi, mauaji ya halaiki. Utakuwa mwisho mambo yote ya kuumiza, huzuni zote, makubwa kwa madogo, ambayo Shetani ametusababishia.

Hakuna Maumivu

Biblia inaahidi kwamba dhambi haitajitokeza tena (angalia Nahumu 1:9). Inasema kuwa Mungu atafanya kila kitu kuwa kipya—pamoja na sisi wenyewe: “Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita” (Ufunuo 21:4).

Je, Mungu anajali kwamba unaumia? Kwa hakika anajali. Je, atafanya jambo fulani kuhusiana na hilo? Kwa hakika anajali—katika hali hiyo kwa ujumla wake na kwako binafsi. Ameahidi, “Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa” (Waebrania 13:5).

<!-- Start of StatCounter Code for WordPress.org (I pay for<!-- [et_pb_line_break_holder] -->the hosting) --><!-- [et_pb_line_break_holder] --><script type="text/javascript"><!-- [et_pb_line_break_holder] -->var sc_project=11587914; <!-- [et_pb_line_break_holder] -->var sc_invisible=0; <!-- [et_pb_line_break_holder] -->var sc_security="4a09a56b"; <!-- [et_pb_line_break_holder] -->var scJsHost = (("https:" == document.location.protocol) ?<!-- [et_pb_line_break_holder] -->"https://secure." : "http://www.");<!-- [et_pb_line_break_holder] -->document.write("<sc"+"ript type='text/javascript' src='" +<!-- [et_pb_line_break_holder] -->scJsHost+<!-- [et_pb_line_break_holder] -->"statcounter.com/counter/counter.js'></"+"script>");<!-- [et_pb_line_break_holder] --></script><!-- [et_pb_line_break_holder] --><noscript><div class="statcounter"><a title="Web Analytics"<!-- [et_pb_line_break_holder] -->href="http://statcounter.com/" target="_blank"><img<!-- [et_pb_line_break_holder] -->class="statcounter"<!-- [et_pb_line_break_holder] -->src="//c.statcounter.com/11587914/0/4a09a56b/0/" alt="Web<!-- [et_pb_line_break_holder] -->Analytics"></a></div></noscript><!-- [et_pb_line_break_holder] --><!-- End of StatCounter Code for WordPress.org (I pay for<!-- [et_pb_line_break_holder] -->the hosting) -->