Rejea kwenye Pumziko

Taarifa za habari, mawasiliano, na burudani katika ulimwenguni wa leo, vyote vinapatikana kwa saa 24 kwa siku, siku 7 kwa juma kupitia mtandao, televisheni na simu.

Kwa baadhi yetu, siku za kazi zenye saa nane hadi tisa zimegeuzwa na kusababisha tufanye kazi kila saa kiasi kwamba hatulali kwa sababu biashara na ulimwengu huvamia nyumba zetu kupitia televisheni, redio, mtandao na simu. Lakini muda sio mrefu tunakuja kutambua kwamba tunahitaji pumziko—siyo kukaa bila kazi kabisa, bali badiliko. Badiliko kutoka hali isiyokoma ya kuhangaikia fedha… na kuelekea katika mambo yale yasiyokoma ambayo ni ya milele. Badiliko, naam, kurejesha upendo, na uhusiano wa familia, na mahali petu ulimwenguni. Mwanafalsafa mashuhuri aitwaye Socrates alisema “Maisha yasiyofanyiwa tathmini hayafai kuyaishi,” na kwa kiwango kikubwa tunalifahamu hili kuwa sahihi. Tunafanya kazi na kupanga, tunajitahidi na kujipatia vitu, lakini kwa ajili ya lengo gani? Kwa kadiri tunapojiruhusu sisi wenyewe kunaswa na habari zisizokoma zitokanazo na magazeti, redio, televisheni, mtandao na simu zetu, hatutaweza kutulia na kutafakari masuala ya msingi kabisa.

Imefikia hatua ambayo machapisho ya kibiashara kama vile Jarida la Wall Street hutoa wito kwa kusema—je unaweza kuliamini hilo?—kurejea kwenye Sabato. Tahariri iliyotolewa mnamo mwezi June 15, 2007 iitwayo, “The Decline of the Sabbath” (Kuhafifia kwa Sabato) ambayo iliandikwa na Mollie Ziegler Hemingway inaliweka jambo hilo kwa namna hii: “Upande mwingine wenye madhara katika mafanikio tunayoyafurahia ni kwamba tumepoteza siku yetu ya pumziko kwa kuingiza badala yake siku nyingine ya utumiaji. Hatua za maendeleo ya haraka ya biashara na teknolojia zimeleta chaguzi zisizotegemewa kabisa zinazosababisha kupuuzia familia, dini na pumziko—siyo tu katika siku ya Sabato lakini katika kila siku za juma.

Sabato hutupatia dawa hasa tunayoihitaji ili kuzuia mwingiliano wa taarifa nyingi zilizopita kiasi pamoja na hofu. Sabato hutupatia kimbilio, pumziko, na likizo fupi ya kuondokana na shughuli tunazokumbana nazo wakati wote na vizuizi visivyokoma vya ‘habari.’

Biblia inatuambia kuwa Mungu aliumba uhitaji wetu wa pumziko—na tiba yake—katika mpango wa Uumbaji. “Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi Yake yote aliyoiumba na kuifanya.” Kwa kitendo Chake cha kupumzika kwa kuacha shughuli zote alizokuwa amefanya, Mungu hutupatia kielelezo muhimu. Katika Amri Kumi, huufanya mfano huu kuwa dhahiri na wa lazima: “Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako.” Zingatia kuwa haya mafungu mawili ya Biblia hayasemi, “fanya kazi kwa muda wa siku sita kati ya saba, halafu pumzika katika siku mojawapo.” Badala yake, ni dhahiri kuwa siku ya saba ni Sabato. Siku ya saba, na wala siyo siku yoyote ya saba. Na siku hiyo ni Jumamosi.

Jumamosi? Inawezekana kwamba umewahi kufundishwa kwamba Sabato ya Jumamosi ilitolewa pale Sinai kwa ajili ya Wayahudi peke yao. Kama hilo ni kweli, vivyo hivyo ‘kutoua’ na ‘kutoiba’ vingelikuwa vilevile kwa ajili ya Wayahudi peke yao. Au unaweza kuwa umesikia kwamba msalaba ulibatilisha na kuondoa masharti ya Sabato. Kwa mara nyingine tena, hilo lingemaanisha tuko huru kuua na kuiba—lakini hakuna mtu yeyote anayeamini hilo. Inawezekana umewahi kufundishwa kwamba tunaabudu katika siku ya Jumapili ili kuuheshimu ufufuo wa Bwana. Kwa hakika hilo ni tukio la msingi kulikumbuka. Lakini Biblia kamwe haituambii kuukumbuka ufufuo Wake, bali tunaambiwa kukumbuka kifo Chake (1 Kor. 11:26).

Tunaambiwa ‘kukumbuka’ mauti Yake, jambo ambalo hutupatia mfanano wa kushangaza wa namna Amri Kumi zinavyotuambia ‘kuikumbuka’ Sabato. Na tunagundua kuwa siku pekee nzima ambayo Yesu alipumzika kaburini ilikuwa—Sabato. Badala ya kuondoa Sabato, kifo cha Yesu huithibitisha. Kama alivyokuwa amepumzika katika kazi ya uumbaji katika siku ya saba ya juma lile la Uumbaji, Yesu alipumzika kwa kuiacha shughuli Yake ya ukombozi katika siku ya saba ya juma la ukombozi (juma alilokufa kwa ajili ya dhambi zetu).

Kwa kweli, wengi wetu hatupendi dhana zinazohusiana na “amri” au “utii.” Lakini katika suala hili hasahasa, huko ni kutokuwa na busara. Hebu fikiria endapo daktari alikuambia kuchukua likizo fulani, na kisha akabainisha kwamba alikuwa amechukua likizo iliyokusudiwa kutimiza mahitaji yako ya dhati. Hivyo ndivyo Sabato ilivyo. Yesu mwenyewe alisema, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya Sabato.” Hilo lina maana kwamba Sabato siyo sheria tu isiyokuwa na kusudi lolote, lakini badala yake ni pumziko lililokusudiwa kutimiza mahitaji yetu.

Lakini kwa nini siyo Jumapili, au Jumanne? Kwa nini Jumamosi? Kumbuka kuwa kisa cha uumbaji katika kitabu cha Mwanzo kilituambia kwamba “Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa.”

Kitendo cha “kutakasa kitu fulani” humaanisha nini? Musa aliposimama mbele ya kile kichaka kilichowaka moto, alisimama katika ardhi takatifu. Ni nini kilichopafanya kuwa patakatifu? Uwepo wa Mungu. Mungu huifanya Sabato kuwa takatifu kwa kuwepo katika siku hiyo katika namna fulani maalumu.

“Hebu ngoja kidogo,” unaweza kusema: “Lakini si Mungu yuko kila siku?” Na kwa kweli, hilo ni sahihi. Lakini ni sahihi vilevile kuwa Mungu yuko kila mahali—lakini Musa hakutakiwa kuondoa viatu vyake alipokuwa kila mahali, lakini tu katika eneo lile ambako kichaka kilikuwa kikiwaka moto. Kwa sababu, kama ilivyo kwa Sabato, Mungu alikuwepo katika eneo la kichaka hicho kwa namna fulani iliyotofautiana na namna alivyo kila mahali kwingineko. Na wale wanaoitenga Sabato, siku ya saba, ili kupumzika kwa kuacha shughuli zao za kila siku na kukutana na familia zao na kukutana na Mungu pia, wanaweza kutoa ushuhuda kwamba kwa hakika Mungu anaweza kuleta uzoefu wenye mguso kwa namna ya pekee katika siku hiyo.

Kama unahitaji kuchunguza manufaa mbalimbali yatokanayo na utunzaji wa Sabato, kuna watu wanaoishi karibu na wangefurahia kukueleza hilo. Waadventista wa Sabato watakuwa na furaha kukueleza zaidi juu ya hili. Unaweza kupata mambo mbalimbali juu ya hili na habari zingine zinazovutia na zenye manufaa katika mtandao kwenye tovuti hii: www.glowonline.org.

www.kujifunzabiblia.com

<!-- Start of StatCounter Code for WordPress.org (I pay for<!-- [et_pb_line_break_holder] -->the hosting) --><!-- [et_pb_line_break_holder] --><script type="text/javascript"><!-- [et_pb_line_break_holder] -->var sc_project=11587914; <!-- [et_pb_line_break_holder] -->var sc_invisible=0; <!-- [et_pb_line_break_holder] -->var sc_security="4a09a56b"; <!-- [et_pb_line_break_holder] -->var scJsHost = (("https:" == document.location.protocol) ?<!-- [et_pb_line_break_holder] -->"https://secure." : "http://www.");<!-- [et_pb_line_break_holder] -->document.write("<sc"+"ript type='text/javascript' src='" +<!-- [et_pb_line_break_holder] -->scJsHost+<!-- [et_pb_line_break_holder] -->"statcounter.com/counter/counter.js'></"+"script>");<!-- [et_pb_line_break_holder] --></script><!-- [et_pb_line_break_holder] --><noscript><div class="statcounter"><a title="Web Analytics"<!-- [et_pb_line_break_holder] -->href="http://statcounter.com/" target="_blank"><img<!-- [et_pb_line_break_holder] -->class="statcounter"<!-- [et_pb_line_break_holder] -->src="//c.statcounter.com/11587914/0/4a09a56b/0/" alt="Web<!-- [et_pb_line_break_holder] -->Analytics"></a></div></noscript><!-- [et_pb_line_break_holder] --><!-- End of StatCounter Code for WordPress.org (I pay for<!-- [et_pb_line_break_holder] -->the hosting) -->