Unaweza Kuitumaini Biblia

Biblia ni kitabu cha zamani sana kuliko vyote ulimwenguni, na kimekuwa kitabu kinachosomwa sana ulimwenguni. Vyama mbalimbali vya Biblia ulimwenguni huuza au hugawa nakala zaidi ya milioni 20 kila mwaka.

Kadiri ambavyo wasomi wamelichunguza kwa kina kila neno la Biblia katika kipindi cha miaka elfu nyingi iliyopita na kadiri ambavyo wametafiti kwa uangalifu katika akiolojia ya Biblia na historia na lugha za zamani ambazo zilitumika kuiandika, unaweza kufikiri kuwa mpaka sasa huenda wangekuwa wamefikia mwafaka fulani kuhusu chanzo chake, maana, na kuaminika kwake.

Hata hivyo, kinyume chake ni sahihi. Baadhi ya watu huamini Mungu aliamrisha kila neno la Biblia. Wengine husema si chochote zaidi tu ya mkusanyiko wa visa vya kale na mapokeo. Baadhi huamini kwamba visa vyake ni kumbukumbu yenye historia ya kweli kabisa; wengine huamini kuwa ni mkusanyiko wa visa.

Hivyo, unaweza kuitumaini Biblia? Zifuatazo ni sababu tatu zinazoeleza kwa nini jibu la swali hilo ni ndiyo.

Akiolojia

Katika wakati mmoja au mwingine, watu wanaoishuku Biblia wamehoji uhalisi kihistoria wa karibu kila kisa ndani ya Biblia. Hata hivyo, ushahidi wa akiolojia au elimu ya mambo ya kale umethibitisha kimoja baada ya kingine miongoni mwa visa hivi. Hapa kuna mifano miwili;

Belshaza wa Danieli. Danieli anaarifu kuwa Belshaza alikuwa ni mfalme wa Babeli wakati wa kuangushwa kwa taifa hilo na Waajemi. Hadi kufikia mwishoni mwa miaka ya 1800, orodha zingine zote za wafalme wa Babeli zilizokuwa zimegunduliwa zilieleza kuwa Nabonidus ndiye aliyekuwa mfalme wa mwisho wa Babeli—na kuwafanya wasomi kufikia uamuzi kuwa Belshaza alikuwa ni mhusika wa kufikirika ambaye Danieli alimbuni. Hata hivyo, nyaraka za kale zimedhihirisha kuwa Belshaza alitawala pamoja na Nabonidus, baba yake.

Msomi mmoja alitoa kauli ifuatayo ya kushangaza: “Kati ya kumbukumbu zote zisizokuwa za Wakaldayo zinazohusika na hali iliyokuwepo mwishoni mwa ufalme Babeli Mpya, sura ya tano ya kitabu cha Danieli ni ya pili kwa usahihi baada ya maandishi maalum ya kikabari kadiri ambavyo matukio makuu yanahusika.” (1)

Injili Nne

Kwa kiwango kikubwa, ugunduzi wa akiolojia unaunga mkono kauli za historia zilizotamkwa na waandishi walioandika historia ya maisha ya Yesu. Kwa mfano, Yohana anataja jengo linaloitwa Bethzatha kule Yerusalemu ambamo ndani yake kulikuwa na birika. (2) Uchimbuaji wa mambo ya kale(akiolojia) umevumbua jengo ambalo linaendana kwa usahihi kabisa na maelezo ya Yohana.

Wavumbuzi wa mambo ya kale wamegundua pia kile ambacho huenda ni nyumba ya kifahari ya Kayafa, kuhani mkuu aliyesimamia hukumu ya Yesu katika ile Sanhedrini. (3) Inajumuisha uwanja wa nje, mahali ambapo Petro alimkania Kristo mara tatu, na jumba kubwa kiasi cha kutosha kuendeshea kesi. Akiolojia huonesha kuwa Biblia ni historia ya ukweli sio hadithi za uongo.

Unabii

Imani katika Biblia imethibitishwa pia na sehemu kubwa ya unabii wake, na hasa huu mmoja. Danieli, nabii wa zamani alitabiri kwa usahihi mwaka ambao Yesu alianza huduma Yake. Kwa mujibu wa Danieli 9:25, “Tangu kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hata zamani Zake Masihi [Yesu] Aliye mkuu; kutakuwa na majuma saba; na katika majuma sitini na mawili.” Hii ni jumla ya majuma 69, au siku 483. Wasomi kwa ujumla hukubaliana kuwa majuma ya Danieli yanapaswa yaeleweke kama “majuma ya miaka,” siku ikimaanisha mwaka, kwa jumla ya miaka 483.

Wakaldayo waliiangamiza Yerusalemu na kuchukua sehemu kubwa ya mateka kwenda Babeli. Baadaye, wafalme watatu wa Kiajemi walitoa matamko wakiwaruhusu Wayahudi kurudi kwenye nchi yao. Tamko linalokidhi kwa ukaribu sana matakwa ya unabii wa Danieli ni lile lilitolewa na Atashasta mwaka 457 KK. Hesabu rahisi huonesha kuwa miaka 483 ya Danieli iliishia katika mwaka wa 27 BK.

Yesu alitiwa mafuta kwa ajili ya huduma Yake wakati wa Ubatizo Wake. Kwenye Injili yake, Luka anatupatia taarifa za kina zilizopangiliwa zinazonesha kuwa Yesu alibatizwa mwaka wa 27 B.K. (4) Hivyo, Danieli alitabiri mwaka halisi ambao Yesu angeanza huduma Yake! Huu ni ushahidi wenye nguvu kwamba tunaweza kuitumaini Biblia kama ujumbe kutoka kwa Mungu, sio tu kutoka kwa wanadamu.

Uzoefu binafsi

Ingawa, kwa jinsi akiolojia na unabii zinavyovutia katika kuthibitisha hali ya kutumainika kwa Biblia, ushahidi muhimu kuliko wote ni tofauti ambayo Biblia imeleta katika maisha ya watu wengi sana.

Biblia hutuambia juu ya Mungu anayetupenda, ambaye ni “mwingi wa huruma, mwenye fadhili,… mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi.” (5) Mungu pia hutusaidia kuupata ushindi dhidi ya uraibu na mazoea mabaya ambayo vinginevyo yangeharibu maisha yetu.

Paulo alisema kwamba injili—habari njema kuhusu Yesu—ni “uweza wa Mungu uletao wokovu, kwa kila aaminiye” “ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya Roho.”

Na huu ni ukweli kabisa. Watu ulimwenguni kote wamegundua kuwa wanapoyaweka maisha yao kwa Mungu, huweka ndani yao nguvu ya kuwawezesha kuishi kila siku karibu na maisha halisi ambayo Biblia huendelea kuyahimiza kwa ajili yao. Huo ni ushahidi mkubwa kabisa kwamba, Naam, unaweza kuitumaini Biblia.

Namna ya Kuielewa Biblia

Kama huifahamu Biblia, mapendekezo yafuatayo yatakusaidia kuielewa.

• Soma visa vya Biblia. Visa vingi vya Biblia hupatikana kwenye vitabu kadhaa. Vitabu vya visa vya Agano la Kale hujumuisha Mwanzo, Kutoka (nusu ya kwanza), Yoshua hadi Esta, na Danieli. Katika Agano Jipya, visa vinapatikana katika Mathayo, Marko, Luka, Yohana, na Matendo. Usomaji wa sehemu hizi za Biblia mara nyingi utakufanya uwe na uelewa mzuri juu ya kitu gani kilitokea lini.

• Soma kwa ajili ya ukuaji kiroho. Masomo muhimu zaidi katika Biblia ni ya kiroho. Kadiri unavyosoma, basi, angalia namna ambayo mafundisho ya Biblia yanaweza kukufanya uwe mwenye huruma, mwenye haki, na mwaminifu.

• Soma kwa maombi. Waandishi wa Biblia waliiandika chini ya uongozi wa Mungu. Kwa sababu Mungu ndiye Mtunzi wa Biblia, anaweza kukusaidia uielewe. Kwa hiyo, omba msaada Wake kila wakati unapoichukua Biblia ili kuisoma.

• Soma kwa utaratibu bila kukoma. Anzisha tabia ya kusoma sehemu ya Biblia yako kila siku. Pia, maduka mengine ya vitabu vya Kikristo yana miongozo ya kujifunzia Biblia itayokusaidia kuelewa kile ambacho Biblia humaanisha.

1) Raymond P. Dougherty, Nabonidus and Belshazzar, 216

2) Yohana 5:2

3) Mathayo 26:57, 58

4) Luka 3:1

5) Kutoka 34:7

 

 

 

<!-- Start of StatCounter Code for WordPress.org (I pay for<!-- [et_pb_line_break_holder] -->the hosting) --><!-- [et_pb_line_break_holder] --><script type="text/javascript"><!-- [et_pb_line_break_holder] -->var sc_project=11587914; <!-- [et_pb_line_break_holder] -->var sc_invisible=0; <!-- [et_pb_line_break_holder] -->var sc_security="4a09a56b"; <!-- [et_pb_line_break_holder] -->var scJsHost = (("https:" == document.location.protocol) ?<!-- [et_pb_line_break_holder] -->"https://secure." : "http://www.");<!-- [et_pb_line_break_holder] -->document.write("<sc"+"ript type='text/javascript' src='" +<!-- [et_pb_line_break_holder] -->scJsHost+<!-- [et_pb_line_break_holder] -->"statcounter.com/counter/counter.js'></"+"script>");<!-- [et_pb_line_break_holder] --></script><!-- [et_pb_line_break_holder] --><noscript><div class="statcounter"><a title="Web Analytics"<!-- [et_pb_line_break_holder] -->href="http://statcounter.com/" target="_blank"><img<!-- [et_pb_line_break_holder] -->class="statcounter"<!-- [et_pb_line_break_holder] -->src="//c.statcounter.com/11587914/0/4a09a56b/0/" alt="Web<!-- [et_pb_line_break_holder] -->Analytics"></a></div></noscript><!-- [et_pb_line_break_holder] --><!-- End of StatCounter Code for WordPress.org (I pay for<!-- [et_pb_line_break_holder] -->the hosting) -->