Vita Mbinguni
Hivi unajua kwamba imeandikwa kuwa vita vya kwanza kabisa kuwahi kupiganwa vilifanyikia mahali ambapo usingeliweza kupategemea? Biblia hutuambia kuwa “kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni.” Ufunuo 12:7-8. Vita hivi vilianzaje na vilihusu nini? Jibu la maswali haya hudhihirisha sababu iliyo chimbuko la matatizo yote duniani, pamoja na ndani ya moyo wa mwanadamu.
Nabii Ezekieli hutupatia taarifa ya vita hivi vya kwanza na uasi wa Shetani dhidi ya Mungu. Lusifa, anayetajwa kama “kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye,” alikuwa “mkamilifu” alipoumbwa “hata uovu ulipoonekana ndani” yake. Ezekieli 28:14-15. Nafasi hii ya kerubi (au malaika) afunikaye hudhihirisha mambo mengi kuhusu uasi wa Lusifa. Katika Agano La Kale, Mungu alikuwa amewapatia wana wa Israeli kielelezo cha chumba chake cha kiti cha enzi Mbinguni kinachoitwa patakatifu (Angalia Kutoka 25:8). Paulo anaandika kuwa patakatifu hapa duniani palikuwa ni kielelezo cha “mambo ya mbinguni.” Waebrania 8:5. Ndani yake mlikuwa na chumba maalumu kinachoitwa mahali patakatifu mno palipokuwa na Sanduku la Agano lenye Amri Kumi ndani yake. Juu ya Sanduku hili palikuwa na “kiti cha rehema” na pande zote mbili za kiti hiki cha rehema palikuwa na “kerubi” “afunikaye kiti cha rehema” na “afunikaye sanduku” hilo. Angalia Kutoka 25:16-22; 1 Wafalme 8:7.
Hii huonesha kwamba kiti cha enzi cha Mungu ni kiti cha rehema na msingi wake, na ufalme wake ni sheria yake. Lusifa, aliyekuwa hapo kwanza “kerubi afunikaye,” aliwajibika kwa kuiinua na kuilinda au “kuifunika” sheria hii. Hata hivyo, uasi ukaanza kwa sababu “udhalimu” au dhambi ilionekana ndani ya Lusifa. Na dhambi ni nini? “Dhambi ni uasi wa sheria.” 1 Yohana 3:4. Lusifa, aliyepaswa kuitetea sheria ya Mungu, ule msingi wa serikali ya mbinguni, aliiasi dhidi ya sheria hiyo. Kama matokeo yake, kulikuwa na vita mbinguni.
Lakini Lusifa alikuwa na hoja gani dhidi ya sheria? Angalia hoja nyingine yenye nguvu katika pambano hili ulioandikwa na nabii Isaya. “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu…Nitafanana na Yeye Aliye juu.” Isaya 14:12-14. Lusifa aliwasilisha hoja kuwa angekuwa “kama Mungu,” ikimaanisha, katika haki, kuwepo na haja ya kutii sheria ya Mungu. Alidhani angeweza kujiaamulia mwenyewe lililo jema na lililo baya. Kwa maneno mengine, uasi wa Lusifa ulitokana na kujihesabia haki mwenyewe. Alikuwa akidai kuwa sheria ilikuwa inawabana na kwamba malaika huru wenye akili na utashi hawakuhitaji utawala kama huo. Hoja hii ilidanganya idadi kubwa ya malaika. Malaika hawa na Lusifa walitupwa kutoka Mbinguni, pamoja na chuki yao dhidi ya sheria.
Kwa maelezo haya tunaweza kuelewa vyema kwa nini dunia na moyo wa mwanadamu mara nyingi hupata matatizo. Hata leo bado Shetani anaichukia sheria ya Mungu, ambayo ni msingi wa serikali ya Mungu. Mungu anawatafuta watu kwa ajili ya ufalme wake, lakini lazima wawe tayari kuzishika sheria za Mbinguni. Huu ni ukweli unaofanana kwa serikali yoyote.
Shetani alipomwendea Adamu na Hawa katika ile bustani, aliwajaribu kwa udanganyifu huo. Mnaweza kuwa “kama Mungu” bila kumtii. Mwanzo 3:1-4. Udanganyifu huo huo uliosababisha anguko la malaika mbinguni, ulisababisha anguko la Adamu na Hawa katika bustani ya Edeni. Na kama vile malaika walivyotupwa kutoka mbinguni, ndivyo Adamu na Hawa walivyoondolewa kutoka katika bustani ya Edeni. “Kwa hiyo Bwana Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa. Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima. Mwanzo 3:23-24. Adamu na Hawa waliruhusu akili zao zibadilishwe na Shetani. Sasa walikuwa na “nia ya mwili,” ambayo Paulo anaandika juu yake akisema, “ni mauti;… Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.” Warumi 8:7-8.
Lakini Mungu asingemwacha mwanadamu aangamie. Angemtuma Mwanawe kuja ulimwenguni. Wanadamu wangepata nafasi ya pili. Ili kuingia katika ufalme wa mbinguni, lazima mwanadamu kwa mara nyingine tena atii sheria za mbinguni. Kwa hiyo Paulo anaandika, “Na Roho Mtakatifu naye amshuhudia; kwa maana, baada ya kusema, Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, Na katika nia zao nitaziandika; ndipo anenapo, Dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa.” Waebrania 10:15-17.
Matatizo yote duniani na yale yaliyomo katika moyo wa mwanadamu ni matokeo ya kuuamini uongo wa Shetani kwamba mwanadamu hahitaji kutii sheria ya Mungu au kwamba anaweza kuwa mwenye haki pasipo uongozi wa Mungu. Shetani amekwenda mbali kiasi cha kuuficha uongo ndani ya mwonekano wa haki; hili linaonekana kupitia fundisho la wale wanaodai kuwa Wakristo kwamba sheria ya Mungu imekoma, kwamba neema kwa namna fulani hubatilisha hitaji la kutii amri za Mungu. Yohana anaonya dhidi ya udanganyifu huu wa kujihesabia haki anapoandika, “Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua Yeye, ikiwa tunashika amri Zake. Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri Zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani Yake.” 1 Yohana 2:3-4.
Shetani ana hasira dhidi ya wale wasioanguka kutokana na udanganyifu huu. Huenda “zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu.” Ufunuo 12:17.
Biblia hudhihirisha jinsi Shetani atakavyofanya kazi ili kuwadanganya watu kuhusu sheria ya Mungu. Nabii Danieli anaandika kuhusu jaribu la Shetani “kubadili…sheria.” Danieli 7:25. Kwa nini? Kwa sababu Shetani anajua kuwa kupuuzia amri moja ni kuwa na hatia ya kuvunja amri zote. Yakobo 2:10-12.
Kwa kweli Shetani amebadili kwa werevu moja ya Amri Kumi na watu wachache huonekana kulitambua hilo. Amefanyia hili moja kwa moja kupitia ndani ya kanisa. Tunakutia moyo kusoma kwa maombi Amri Kumi kama zilivyoandikwa katika Kutoka 20 na kujaribu kugundua ni amri gani iliyobadilishwa na kuingizwa mafundisho ya wanadamu. Ikiwa Shetani anaweza kuwaongoza Wakristo kupuuzia mojawapo ya Amri za Mungu, kimsingi anawaongoza waishi katika mawazo yake ya upingaji sheria.
Mwishoni kutakuwa na kundi la watu wanaopinga udanganyifu wa yule mwovu na kuthibitisha wenyewe kuwa waaminifu kwa ufalme wa Mbinguni. Hawataiacha sheria ya Mungu. Vita vya kwanza kuwahi kupiganwa vilikuwa dhidi ya sheria ya Mungu (kwa sababu sheria hudhihirisha tabia ya Mungu). Vita vya mwisho duniani vitakuwa dhidi ya jambo hilo hilo. Yohana anaandika juu ya kundi hili litakaloshinda. “Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake.” Ufunuo 22:14. Hebu uwe sehemu ya kundi hilo linaloshinda.