Zawadi Kwa Ajili Yako

 

Mlio wa simu—wito ambao kila mtu aliungojea, na ambao kila mtu aliuogopa—uliita saa 8:00, usiku wa manane. “Tumepata moyo kwa ajili ya Brody*,” sauti ilisema. Kila mmoja alikuwa akitarajia ile simu kwa sababu Brody, mwenye umri wa miaka 12, alikuwa kwenye orodha ya wanaosubiri kupandikizwa moyo kwa siku nyingi, na muda si mrefu afya yake ingekuwa mbaya na asingeweza tena kupandikizwa moyo. Kama ingetokea hivyo angeondolewa kwenye orodha na angepoteza tumaini lake la mwisho. Lakini katika siku hii, Brody na familia yake walikuwa wanakaribia kupokea zawadi ya pekee—zawadi ya moyo mpya, zawadi ya maisha mapya.

Biblia hutwambia kuwa sisi sote tuko kwenye hali ya kukata tamaa zaidi kuliko hali ya Brody, kwa maana zaidi ya maisha haya ya sasa yako hatarini. Tumestahili kifo cha milele, kwa sababu “mshahara wa dhambi ni mauti” (Warumi 6:23), na “kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu” (Warumi 3:23). Tunapoelewa lugha ya asilli ya Kiyunani katika fungu la mwisho, tunatambua jinsi hali yetu ilivyo ya kukata tamaa. Neno la Kiyunani lililotafsiriwa kama “kupungukiwa” huonesha tendo endelevu—tunaendelea kupungukiwa utukufu. Dhambi haihusu tu matendo ya zamani, bali inahusu hali yetu endelevu ya kuishi.

Wakati mambo yanapotuendea vizuri, ni rahisi kujipatia tumaini kuwa hii haiko hivyo. Kwamba sisi ni watu wema hasa—sio wakamilifu, kumbuka—lakini sio waovu sana. Na wakati jirani anapopandishwa cheo kazini na nyongeza ya mshahara tuliyokuwa tunatarajia, au anaponunua gari jipya, hapo ndipo tunapogundua wivu mioyoni mwetu. Au tunamwona mwanamke mzuri sana ambaye sio mke wetu kwenye TV, kwenye filamu au mahali pengine na kushangaa…. ndiyo, hebu tuseme tu kuwa tamaa hufanya uwepo wake ujulikane. Huenda mtu fulani anaendesha gari lake na anatutendea mabaya tunapokuwa kwenye foleni ya magari, na tunagundua kiwango fulani cha hasira kinachotushangaza. Kadri tunavyoyachunguza maisha yetu kwa umakini, ndivyo tunavyoona kuwa hii ni kweli.

Kama vile kijana asiyeamini juu ya uwepo wa Mungu, na Profesa katika Chuo Kikuu cha Oxford alivyouelezea uzoefu huu, “Kwa mara ya kwanza nilijichunguza mwenyewe kwa umakini mkubwa wote uwezekanao. Na hapo nilipata majibu yaliyonitisha: mkusanyiko wa tamaa nyingi za mwili, mlundikano mkubwa wa tamaa ya ukuu, hali inayoongezeka ya woga, mlundikano wa chuki. Jina langu lilikuwa legioni.” (C. S. Lewis, Surprised by Joy). Dhambi zote hizi, tunaambiwa, hutoka kwenye mioyo yetu ya dhambi. “Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.” (Luka 6:45). Ni kweli, ni mioyo yetu ya dhambi ambayo inaficha hali yetu ya dhambi kutoka kwetu, kwa sababu “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha” (Yeremia 17:9).

Hivyo tunagundua kwamba, kama vile Brody, mioyo yetu ni chanzo cha matatizo yetu. Hatutaweza kupata nafuu. Hakuna dawa wala matibabu yatakayotusaidia—mioyo yetu yenye kasoro lazima ibadilishwe la sivyo tutakufa. Brody alitakiwa kujiorodhesha na kusubiri. Hakuna kiasi chochote cha pesa ambacho kingeweza kununua kile alichohitaji. Kama kusingekuwepo hata mmoja ambaye angempatia moyo, angekufa.

Hali yetu ni sawa na yake, lakini Biblia ina habari njema kwetu sisi sote tuliopo kwenye hali hii ya kukata tamaa. Hutuambia kwamba zawadi hiyo inapatikana. “Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama” (Ezekieli 36:26).

Hata jambo lililo bora zaidi hapa, ni kwamba hakuna kupanga foleni, moyo huu wa kubadilishiwa unapatikana haraka, na mara unapochukua nafasi ya moyo wetu wa zamani, hatutaendelea tu kuishi, tutafurahia maisha tofauti yenye ubora wa hali ya juu.

Katika familia ya Brody kila mmoja alisubiria kwa hofu simu iite kwa sababu mchakato huo ulihusisha hatari kubwa sana. Kabla moyo wenye afya haujapandikizwa, moyo wake ulipaswa kuondolewa. Mara upasuaji unapoanza, kusingekuwa na kurudi nyuma. Wakiwa na mawazo haya yote kwenye akili zao, Bill na Jill waliamka asubuhi na mapema kabla jua halijachomoza, wakajiandaa na kumwandaa pia Brody kwa ajili ya safari muhimu kwenda hospitalini. Walipofika pale, walimwona kijana wao akisukumwa kwenye kitanda cha wagonjwa kwa ajili ya kwenda kwenye chumba cha upasuaji.

Nasi, pia, lazima tupitie aina fulani ya kifo kwanza. Kama vile Brody alivyotakiwa kuwaruhusu madaktari wa upasuaji kuuondoa moyo wake kabla ya kupandikiza mwingine, hivyo ndivyo tunavyolazimika kuuondoa moyo wetu wa asili. Lazima tutambue kwamba tunahitaji zaidi ya mguso mmoja hapa na pale, zaidi ya marekebisho madogo au masahihisho—tunahitaji upasuaji makini kabisa. Hakuna lolote pungufu ya hapo litakaloweza kusaidia.

Hatari hii ya kuogopesha ndiyo iliyomfanya Brody na familia yake kutishwa na wito wa ile simu kwamba moyo umepatikana. Na ingawa wazazi wa Brody walifurahia fursa ya maisha bora kwa mtoto wao, uhalisia mwingine wa kuhuzunisha uliingia. Waligundua kuwa tukio lilelile lililowapatia tumaini jipya lilikuwa limeondoa matumaini ya familia nyingine fulani. Bahati ya Brody ya kuishi ilikuja kwa gharama ya kifo cha mtu mwingine.

Fursa yetu kwa ajili ya kupandikizwa moyo wa kiroho, kwa ajili ya wokovu toka dhambini, kwa ajili ya maisha bora ya hapa na sasa hivi, na maisha ya milele baada ya hapa, pia huja kwa gharama ya kupoteza maisha. “Bali Mungu aonyesha pendo Lake Yeye Mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi” (Warumi 5:8). Angalia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sio “tulipokuwa tunastahili,” au “tulipoitii sheria ya Mungu kikamilifu,” au hata “tulipotambua hitaji letu,” lakini “tulipokuwa tukingali wenye dhambi.”

Moyo wa Brody ungeendelea tu kuwa na hali mbaya ikiwa usingebadilishwa. Hitaji lake kuu lilimfanya astahili. Na alipaswa kumtegemea mtu mwingine, mahali fulani, anayetoa zawadi ya moyo wenye afya. Hakuna mioyo iliyokuwa inauzwa, na kama ingekuwepo, yeye na familia yake wasingemudu kununua. Kwa mara nyingine tena, hali hiyo inafanana na jinsi ukombozi ulivyo: “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu” (Warumi 6:23). Hivyo tunaona kwamba fungu hilohilo linalotuonya kwamba tumejipatia kifo, pia hututangazia dawa kama zawadi.

Zawadi kubwa kabisa, ya thamani zaidi katika umilele wote. Hatuhitaji kujiorodhesha, hatupaswi kusubiri. Tunaweza kuipata hapa na sasa hivi, kwa kuiomba tu. Tumeziona hatua za kuipata. Tambua tu hitaji lako, kiri kwamba unauhitaji moyo huu mpya, na mwombe Mungu akupatie. Hakuna kanuni ya kimwujiza, hakuna maneno maalumu ya kutumia. Omba tu. Brody alitoka kwenye upasuaji wa kupandikizwa moyo akiwa mwenye furaha. Siyo tu kwamba alikuwa na moyo mpya, alikuwa na maisha mapya. Lakini alipaswa kujifunza jinsi ya kuishi maisha haya mapya. Tunapopokea moyo wetu mpya, sisi pia tunapaswa kujifunza jinsi ya kuishi maisha mapya. Mungu ametupatia kanisa, jamii ya watu wengine ambao wamepokea mioyo mipya, ili watusaidie kujifunza kuishi maisha hayo mapya. Unaweza kupata msaada wa kutafuta moyo mpya, na kulitafuta kanisa, kwa kuingia kwenye tovuti ya www.glowonline.org. Furahia zawadi.

Zawadi Kuu kuliko Zote

Mpango wa ukombozi wetu halikuwa wazo lililojitokeza baadaye bila kutazamiwa, mpango ulioandaliwa baada ya anguko la Adamu. Bali ulikuwa ufunuo wa “siri iliyositirika tangu zamani za milele” (Warumi 16:25). Ulikuwa ufunuo wa kanuni ambazo tangu nyakati zote za umilele zimekuwa msingi wa kiti cha enzi cha Mungu. Tangu mwanzo, Mungu na Kristo walifahamu uasi wa Shetani, na pia walijua anguko la mwanadamu kupitia nguvu ya udanganyifu wa yule mwasi. Mungu hakukusudia kwamba dhambi iweze kutokea, bali aliona uwepo wake hata kabla ya kutokea kwake, na akaandaa njia ya kupambana na hali hii hatari na ya kutisha. Upendo wake kwa ulimwengu ulikuwa mkuu sana, kiasi kwamba alifanya agano ili kumtoa Mwanawe pekee mpendwa, “ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yohana 3:16).

Hili lilikuwa kafara ya hiari. Yesu angeliweza kubaki pamoja na Baba. Angeliweza kubaki na utukufu wa mbinguni, na heshima kuu ya malaika. Bali alichagua kurudisha fimbo utawala mikononi mwa Baba, na kushuka chini kutoka kwenye kiti cha enzi cha ulimwengu, ili aweze kuleta nuru kwa walioingiwa na giza, na uhai kwa wanaoangamia.

Kwa maisha na mauti Yake, amefanikisha hata zaidi ya kurejesha kutoka kwenye uangamivu ulioletwa kwa njia ya dhambi. Lilikuwa lengo la Shetani kuleta utengano wa milele kati ya Mungu na mwanadamu; lakini katika Kristo tunaunganika na Mungu kwa ukaribu zaidi kuliko vile ambavyo tungekuwa iwapo kamwe hatukuanguka dhambini. Katika kuchukua asili yetu, Mwokozi amejifunga Mwenyewe kwa jamii ya wanadamu kwa kifungo ambacho kamwe hakiwezi kuvunjwa. Katika nyakati zote za umilele ameungamanishwa nasi. “Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee” (Yohana 3:16).

Kazi ya ukombozi itakuwa imekamilika. Katika mahali ambapo dhambi ilizidi, neema ya Mungu huzidi sana. Dunia yenyewe, mahali hasa ambapo Shetani hudai kuwa yake, siyo tu kwamba patakombolewa bali pia patatukuzwa. Ulimwengu wetu mdogo, ulio chini ya laana ya dhambi, doa moja jeusi katika umbaji Wake tukufu, utapewa heshima zaidi ya malimwengu mengine yote katika uumbaji wote wa Mungu. Mahali hapa, ambapo Mwana wa Mungu alikaa katika ubinadamu; mahali ambapo Mfalme wa utukufu aliishi na kuteseka na kufa, mahali hapa, atakapofanya mambo yote kuwa mapya, maskani ya Mungu yatakuwa pamoja na wanadamu, “Naye atafanya maskani Yake pamoja nao, nao watakuwa watu Wake. Naye Mungu Mwenyewe atakuwa pamoja nao, [na kuwa Mungu wao].” Na katika kipindi chote cha umilele yote usiokoma kadiri waliokombolewa watakapokuwa wakitembea katika nuru ya Bwana, watamtukuza kwa ajili ya Zawadi Yake isiyoelezeka—Immanueli, “Mungu pamoja nasi.”

*Majina yote katika kisa hiki yamebadilishwa.

 

<!-- Start of StatCounter Code for WordPress.org (I pay for<!-- [et_pb_line_break_holder] -->the hosting) --><!-- [et_pb_line_break_holder] --><script type="text/javascript"><!-- [et_pb_line_break_holder] -->var sc_project=11587914; <!-- [et_pb_line_break_holder] -->var sc_invisible=0; <!-- [et_pb_line_break_holder] -->var sc_security="4a09a56b"; <!-- [et_pb_line_break_holder] -->var scJsHost = (("https:" == document.location.protocol) ?<!-- [et_pb_line_break_holder] -->"https://secure." : "http://www.");<!-- [et_pb_line_break_holder] -->document.write("<sc"+"ript type='text/javascript' src='" +<!-- [et_pb_line_break_holder] -->scJsHost+<!-- [et_pb_line_break_holder] -->"statcounter.com/counter/counter.js'></"+"script>");<!-- [et_pb_line_break_holder] --></script><!-- [et_pb_line_break_holder] --><noscript><div class="statcounter"><a title="Web Analytics"<!-- [et_pb_line_break_holder] -->href="http://statcounter.com/" target="_blank"><img<!-- [et_pb_line_break_holder] -->class="statcounter"<!-- [et_pb_line_break_holder] -->src="//c.statcounter.com/11587914/0/4a09a56b/0/" alt="Web<!-- [et_pb_line_break_holder] -->Analytics"></a></div></noscript><!-- [et_pb_line_break_holder] --><!-- End of StatCounter Code for WordPress.org (I pay for<!-- [et_pb_line_break_holder] -->the hosting) -->